NA WAANDISHI WETU
Mawaziri watano �wala kiapo� hadharani
Waahidi miradi 51, vikiwamo viwanda vitano
Spika apeleka Tume Mtwara kuchunguza
Serikali imejifunga kitanzi kwa wakazi wa mkoa wa Mtwara kutokana na kuahidi kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani humo ikiwa ni njia ya kufikia mwafaka wa mgogoro wa gesi.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliyeongoza ujumbe wa timu ya mawaziri wengine wanne kuzungumza na wananchi hao, jana alikiri kuwa serikali haikuwa na utaratibu mzuri wa kuwahusisha wananchi katika mpango mzima wa usafirishaji wa gesi kwa njia ya bomba kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.
Pinda aliwaeleza wawakilishi wa makundi mbalimbali wakati wa mkutano wa majumuisho ya ziara yake iliyoanza Jumapili mkoani humo kwa lengo la kufikia suluhu kuwa hali hiyo ilisababisha migogoro na vurugu mkoani Mtwara.
Waziri Mkuu ambaye alikutana na wawakilishi hao katika ukumbi wa Veta kuwa tatizo kubwa lililojitokeza katika mpango mzima wa usafirishaji gesi ni serikali kutowaelewesha wananchi wa Mtwara jinsi fursa ya gesi itakavyoendeshwa na kusimamiwa kikamilifu katika kuwaletea maendeleo pamoja na mikoa mingine ya kusini ambayo ndiyo inaonekana bado kuwa nyuma kimaendeleo.
“Katika hili naweza kukiri kuwa serikali ndiyo ilikuwa tatizo…na tatizo lenyewe ni kutowahusisha na kuwaeleza wananchi mikakati yote na fursa zitakazopatikana katika kuinua uchumi wa nchi na wakazi wa maeneo gesi ilipogundulika,” alisema Waziri Pinda.
Pinda aliwataka wananchi wa Mtwara na Watanzania wote kuwa watulivu na waelewa ili Tanzania kwa ujumla inufaike na fursa zinazopatikana nchini.
Aliongeza kuwa tangu walipogundua visima hivyo miaka mitatu iliyopita, kumekuwa na msisimko mkubwa wa watu na kampuni zaidi ya 18 zinazotafuta gesi katika maeneo hayo mpaka sasa kutokukata kutafuta gesi ama mafuta na kwamba hali hiyo inadhihirisha kuwa ni eneo zuri.
Waziri Mkuu aliwaondoa hofu wakazi wa Mtwara na kuwaeleza kuwa gesi itakayosafirishwa ni iliyosafishwa tofauti na walivyokuwa wakielewa awali.
Pinda alisema kuwa kila kitu kitafanyika Mtwara na kwamba kiwanda cha kusafisha gesi ghafi kitajengwa katika kijiji cha Madimba katika wilaya ya Mtwara Vijijini pamoja na vinu vya ufuaji wa gesi, hivyo wakazi wa Mtwara waondoe hofu.
“Ninachowaomba Wana-mtwara ni kuwa wavumilivu, waondoe hofu waliyonayo, nawaahidi kila kitu kitafanyika Mtwara,” alisema na kuongeza: “Usafishaji na ujenzi wa mtambo vitafanyika katika kijiji cha Madimba na hata mabaki ya gesi ghafi yatabaki Mtwara kwa shughuli zingine, na si hilo tu kutakuwepo na ujenzi wa viwanda vingi tu kama tulivyoahidi tangu awali.”
Waziri Pinda alibainisha kuwa ukanda wa kusini ni ukanda ambao unaweza kuunganishwa na nchi nyingine na masoko ya nje na ukasaidia kukua kwa uchumi wa nchi.
AHADI ZA SERIKALI
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Joyce Mapunjo, alisema kuwa jumla ya miradi 51 ya uwekezaji inategemewa kuwekezwa mkoani hapa huku akiwataka wananchi kuuendeleza hali ya amani na utulivu kwa ajili ya uwekezaji huo mkubwa.
Alisema pia kuwa miradi mingine itakayotekelezwa haraka ni ujenzi wa kiwanda cha saruji, kiwanda cha mbolea, kiwanda cha plastiki na kiwanda cha kusindika korosho.
Aidha Mapunju aliitaja miradi hiyo kuwa wa kilimo, mradi wa utangazaji, mradi wa utalii na mradi wa huduma kwa wawekezaji.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo na Makazi, Profesa, Anna Tibaijuka, alisema kuwa katika mpango wa upanuzi na uendelezwaji wa mji wa Mtwara, kata sita zimetengwa kwa ajili ya upanuzi wa mji huo.
“Katika kuhakikisha kwamba tunaendana na mazingira ya sasa ya mji huu na uwekezaji huu mkubwa tunatarajia kufikia hapa, tayari kata sita zimetengwa kwa ajili ya upanuzi wa mji huu wa kisasa ambao serikali unauangalia kama mji wa uwekezaji,” alisema Tibaijuka.
Tibaijuka alizitaja kata hizo kuwa ni Ziwani, Msanga Mkuu, Mbawala, Nanguruwe Naumbu pamoja na Mayanga.
Naye Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, aliwataka wananchi wa mkoani hapa kuacha mara moja vurugu za aina yoyote na kwamba yeye pamoja na wizara yake hawatawavumilia watu ambao wataendelea kuharibu mali na kuwapiga askari.
“Inakera sana kuona askari wakipigwa, inauma sana askari ambaye ni mlinzi wa raia na mali zao akiharibiwa mali zake, wizara yangu haipo tayari kuendelea kuona vurugu za aina yoyote ile zikiendelea, tupo tayari kuzima vurugu hizo kwa kasi ya ajabu na tumejipanga kikamilifu katika kudhibiti aina yoyote ya uhalifu,” alisema.
Aliongeza: “Hii inakatisha tamaa hata kwa watoto wetu ambao wana moyo wa kujiunga na Jeshi la Polisi kutokana na vitendo vya baadhi ya raia kuwashambulia askari wetu, mimi nina miaka 41, kama nitaruhusu hawa watu wachache kupiga raia na kuharibu mali zao, ina maana nimeshindwa kazi na wataniharibia kazi, nipo tayari kupambana na kila aina ya uhalifu.”
Waziri wa Uchukuzi Harrison Mwakyembe alifafanua kuwa, wizara hiyo imejipanga katika kuhakikisha inaendeleza bandari ya Mtwara, kujenga uwanja wa kisasa wa ndege, pamoja na kujenga reli itakayotoka Mtwara, Liganga Mchuchuma hadi Mbambabei.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, aliwataka wazazi wa mkoa huo kuhakikisha kuwa wanawahimiza watoto wao kuzingatia zaidi masomo yao ili kunufaika na fursa mbalimbali za uwekezaji zinazojitokeza mkoani humo.
“Mwaka jana ni wanafunzi 26,287 waliohitimu elimu ya msingi, lakini wanafunzi waliofaulu ni 13,174, mpaka sasa naambiwa wanafunzi 2,223 tu ndiyo walioripoti shuleni, inasikitisha sana na fursa kama hizi watoto wenu watazikosa kwa sababu hawatakuwa na elimu, ” alisema Dk. Kawambwa.
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, alisema mradi wa upanuzi wa banadari ya Mtwara upo mbioni kuanza sambamba na uwanja wa ndege ambao utagharimu Sh. bilioni 32. Dk. Mwakyembe alisema uwanja huo utakuwa na ukubwa sawa na wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) na kwamba utatumiwa na ndege za kubeba abiria hadi 150.
Aliongeza kuwa itajengwa reli kutoka Liganga-Mchuchuna na Mbamba Bay.
Wakati huo huo, Mkuu, Mkuu wa Mkoa huo, Joseph Simbakali, alitumia nafasi hiyo kuwaomba radhi wananchi wa Mtwara kwa kuwaita wapuuzi.
“Naombeni radhi wananchi wote wa Mtwara nilikuwa nimeghafilika, mimi ni binadamu kama binadamu wengine, nilikuwa nimewakosea nawaahidi kuwatumikia, kuwasikiliza wananchi wa Mtwara.” alisema Simbakalia wakati akimkaribisha Pinda.
BUNGE LAJITOSA
Bunge limeingilia kati mgogoro wa gesi na sasa limetangaza kuunda kamati ndogo ya wabunge itakayokwenda mkoani Mtwara kusikiliza maoni na mapendekezo ya wananchi mkoani humo kuhusu gesi na kisha ripoti yake kuwasilishwa bungeni.
Akitangaza azma hiyo bungeni jana, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alisema kamati hiyo pia itazungumza na serikali ili kujua ukweli halisi wa mradi huo wa gesi.
Alisema nia ni kujua kinachoendelea ili wabunge watakapokuwa wanajadili masuala ya gesi ndani ya Bunge wawe na uelewa kuhusu nini hasa kinafanyika kwenye mradi huo.
Alisema wabunge wanapaswa kuwa chombo cha kuleta amani, umoja na hivyo wana fursa nzuri ya kujadili mgogoro wa gesi kwa busara ili kuhakikisha muafaka unapatikana kwa kupitia mazungumzo.
“Najua kuna watu wameanza kuniletea vikaratasi hapa wakiomba suala hili lijadiliwe kwa dharura mimi nakubali, lakini tukijadili kwa dharura ninyi nyote mliosoma magazeti mnalielewa hili suala?” alihoji Spika Makinda.
Alisema kutokana na hali hiyo, meza yake imeona ni busara zaidi kwa Bunge kuunda kamati ambayo itakwenda kuzungumza na wananchi pamoja na serikali ili kujiridhisha na taarifa hiyo itawasilishwa katika Mkutano wa Bunge unaoendelea mjini hapa.
“Tume (kamati) hiyo itakwenda kuwasikiliza wale watu wenyewe na hapo hapo tuisikilize na serikali, tunataka kabla ya kumaliza Bunge hili tuweke nafasi ya kuliongelea humu ndani tukiwa tunajua nini kinachoendelea … nawaomba wenzetu wa Mtwara tume (kamati) yangu itakapokwenda kule iwape ushirikiano,” alisema.
Spika Makinda alisema kwa kuwa kamati itaundwa, suala hilo halitajadiliwa kwa dharura kama baadhi ya wabunge walivyokuwa wanapendekeza. Hata hivyo, alisema wajumbe wa kamati hiyo watatangazwa baadaye wiki hii baada ya kukamilisha kuiunda.
MNYAA: SITAIONDOA HOJA
Akizungumza na gazeti hili, Mbunge wa Mkanyageni, Habib Mohamed Mnyaa (CUF), ambaye amewasilisha kusudio la kuwakilisha hoja binafsi bungeni kuhusu gesi, alisema licha ya kutangazwa kuundwa kwa kamati hiyo ndogo bado hataiondoa hoja yake hiyo.
Alisema ataiondoa hoja hiyo, iwapo mambo yatakayowasilishwa bungeni na kamati hiyo yatafanana na yale aliyonayo.
“Siwezi kuiondoa na asubuhi nimezungumza na Katibu wa Bunge, amesema kuwa ndani ya jambo hili kuna siasa ni lazima Bunge likajiridhisha kwanza kabla ya kuwasilishwa bungeni,” alisema na kuongeza kuwa:
“Hata kama nitabahatika kuingia katika kamati hiyo, sitaondoa hoja yangu hadi hapo nitakapohakikisha kuwa mambo yote niliyonayo yatajumuishwa katika ripoti itakayowasilishwa.”
GHASIA AMNUNIA
“Leo (jana), asubuhi nilimpa mkono wa pole ya kuchomewa nyumba Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Hawa Ghasia, akataa na kuniambia kuwa hapokei mkono wangu kwa nia safi tu,” alisema.
Imeandikwa na Mariam Maregesi, Happy Severine, Mtwara, Restuta James na na Sharon Sauwa, Dodoma.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment