Wakati Nelson Mandela ‘Mzee Madiba’
alipoliongoza taifa la Afrika ya Kusini dhidi ya ubaguzi wa rangi na
kuibuka kuwa miongoni mwa viongozi mashujaa duniani, tunapaswa kujuiliza
ni watu gani katika familia yake ambao walikuwa naye bega kwa bega
wakimuunga mkono muda wote.
Baba yake mzazi alifariki wakati Mandela akiwa na umri wa miaka tisa. Kutoka wakati huo alilelewa na Jonintaba hadi wakati alipoitoroka familia hiyo baada ya kutaka Mandela aoe katika ndoa ambayo tayari ilikuwa imeshapangwa.
Tangu wakati Mandela alipoanza mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi na kutafuta usawa kwa wote, ilitegemewa kuwa mke wake ndiye angekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha mambo yanakwenda sawa. Mandela aliwahi kuwa na wake watatu katika historia ya maisha yake, ambapo mke wa mwisho alimuoa siku alipokuwa akiadhimisha miaka 80 ya kuzaliwa kwake.
Madiba anatajwa kuwa katika kipindi chote cha historia yake amekuwa akiwaunga mkono watoto na upatikanaji wa elimu. Mfuko wa Nelson Mandela wa kusaidia watoto ni sehemu tu ya ushahidi wa mafanikio ya Mandela kuwasaidia watoto.
Mandela ni baba wa watoto sita. Watoto wanne aliwazaa na mke wake wa kwanza, Evelyn Mase na watoto wawili aliwazaa na mke wake wa pili, Winnie Madikizela.
Historia watoto wa Mandela
Wapo kati yao ambao hawakuwahi kwenda kumwona baba yao wakati akiwa gerezani.
Watoto wake wote wawili wa kike aliowazaa na mke wa kwanza walikuwa wakitumia jina la Makazawie. Mtoto wake wa kwanza alifariki akiwa na umri wa miezi tisa na mtoto wa pili alityejulikana kwa jina la Madiba Thembikile (Thembi) alifariki katika ajali ya gari mwaka 1969 akiwa na umri wa miaka 25. Mandela alikuwa gerezani na hakuruhusiwa kwenda kuhudhuria mazishi ya mwanae.
Mtoto mwingine, Makgatho alifariki kwa ugonjwa wa Ukimwi mwaka 2005. Mandela amekuwa mstari wa mbele kupiga vita virus vya HIV na Ukimwi akitumia namba 46664 ambayo ni namba yake alipokuwa gerezani kupiga kampeni.
Mandela na Evelyn walidumu katika ndoa yao kwa miaka 13 kabla haijavunjika mwaka 1957. Evelyn alikuwa muumini wa dhehebu la Mashahidi wa Yehova ambalo lilikuwa haliruhusu waumini wake kushiriki kwenye siasa, hivyo muda wote hakujihusisha na siasa. Alifariki mwaka 2004.
Mandela alimwoa Winnie Madikizera mwaka 1958, ingawa muda mwingi hawakuishi pamoja kwasababu Mandela alikuwa akitumikia kifungo huku Winnie akijijengea umaarufu katika majukwaa ya siasa.
Kutokana na misuguano iliyoibuka ndani ya umaarufu wa kisiasa ya Mandela na winnie walijikuta wakipeana talaka mwaka 1994. Mwaka 1998, Mandela alimwoa Graca Machel ambaye alikuwa mke wa kwanza wa Rais wa Msumbiji.
source: mwananchi